TAARIFA YA UCHUNGUZI WA KIFO CHA MWANDISHI WA HABARI WA CHANNEL TEN BW. DAUD MWANGOSI
1.0 UTANGULIZI
Mnamo tarehe 03 Septemba mwaka 2012, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi (MB) aliteua Kamati ya watu watano kufanya uchunguzi kuhusiana na kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, marehemu Daud Mwangosi, kilichotokea tarehe 02 Septemba 2012, katika Kijiji cha Nyololo,Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa. Kituo cha kazi cha marehemu Daud Mwangosi kilikuwa mkoa wa Iringa ambapo pia alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Iringa (IPC).
Wajumbe wa Kamati hiyo ni:
Jaji (Mst.) Steven Ihema – Mwenyekiti
Bibi Pili Mtambalike – Mjumbe
Kanali (Dkt. Eng) Wema Wilson Wekwe – Mjumbe
Bwana Theophil Makunga – Mjumbe
Naibu Kamishna wa Polisi Issaya Juma. Mngulu – Katibu
Sekretarieti ya Kamati ni:
Bi. Edith T. Assenga – Wizara ya Mambo ya Ndani
Bwana Nasoro H. Msumi – Wizara ya Mambo ya Ndani
2.0 HADIDU ZA REJEA
Kamati ilipewa Hadidu za rejea zifuatazo:
-
Uhalali wa mkusanyiko ulioitishwa na CHADEMA eneo la Nyololo,Wilaya ya
Mufindi, Mkoa wa Iringa tarehe 02 Septemba, 2012 na kuwepo kwa uvunjifu
wa amani.
- Kama yalikuwepo makubaliano au maelekezo kuhusu mikutano ya hadhara au maandamano nchini katika kipindi cha Sensa.
-Mazingira
yaliyosababisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu iliyosababisha kifo cha
Marehemu Daud Mwangosi na wengine kuumizwa, na uwiano wa nguvu hiyo na
tukio.
-Madai
ya kuwepo uhasama kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari Mkoa
wa Iringa na chanzo cha uhasama huo. Aidha kuna madai ya kuwepo kwa
orodha ya waandishi watatu (3) ambao Jeshi la Polisi limepanga
kuwashughulikia.
-Uwepo
wa Sheria, Kanuni au Taratibu zinazotoa uwezo kwa Jeshi la Polisi
kuzuia mikusanyiko inayoitishwa na Vyama vya Siasa na Mamlaka ya Rufaa
endapo vyama hivyo havitaridhika na amri hizo.
-Hali ya Mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa nchini katika Utendaji kazi wao na Utii wa Sheria.
3.0 MUDA WA UCHUNGUZI
Kamati
ilipewa muda wa siku 19 kuanzia tarehe 11 Septemba 2012 iwe
imekamilisha uchunguzi na kuwasilisha Ripoti yake ifikapo tarehe 02
Oktoba 2012.
4.0 NJIA ZILIZOTUMIKA KUFANYA UCHUNGUZI:
4.1 Mahojiano na watu mbalimbali waliokuwepo kwenye tukio.
4.2 Kupitia nyaraka na vielelezo mbalimbali.
4.3 Kutembelea eneo la tukio.
4.4
Majadiliano na vikundi mbalimbali (viongozi wa dini ngazi ya kijiji na
wilaya hadi ya mkoa; viongozi wa vyama vya siasa kwenye ngazi ya kijiji,
wilaya, mkoa na Taifa, viongozi wa serikali ngazi ya kijiji, wilaya,
mkoa, Taifa) na wanakijiji wa Nyololo.
5.0 UCHUNGUZI
Kamati
ya Uchunguzi ilifanya mahojiano na watu mbalimbali ikiwa pamoja na
watendaji wa serikali hususan Kamati za Ulinzi na Usalama ngazi ya
wilaya Mufindi na mkoa wa Iringa viongozi wa Jeshi la Polisi viongozi wa
vyama vya Siasa, Viongozi wa Madhehebu ya Dini, Waandishi wa Habari na
wananchi wa kawaida (ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa).
6.0. YALIYOJITOKEZA
Baada
ya Kamati kukutana na makundi ya watu mbalimbali katika Mkoa wa Iringa
na Viongozi wa Vyama vya Siasa wa kitaifa jijini Dar es Salaam, mambo
kadhaa yalijitokeza na baadhi yao ni:
-Hofu
ya kutoweka kwa amani miongoni mwa viongozi na wananchi hasa katika
mikutano na maandamano ya siasa ambayo yameanza kuota mizizi ya uvunjifu
wa amani na mengine kusababisha mauaji. Viongozi na wananchi wengi
waliotoa maoni yao mbele ya Kamati wameonyesha hofu kuwa hali hiyo
isipodhibitiwa mapema inaweza kulipeleka pabaya Taifa letu.
-Kuna walakini wa mahusiano kati ya waandishi wa habari na Jeshi la Polisi mkoani Iringa.
-Uwepo
wa utashi wa makusudi/dhati kwa viongozi wa vyama vyote vya siasa
kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi ya vyama.
-Umuhimu
wa Ushirikiano na mahusiano baina ya vyombo vya serikali, vyama vya
siasa, wanahabari na wananchi kwa ujumla badala kuonyeshana ubabe ambao
umetufikisha hapo.
- Haja ya kufanya mabadiliko ya kisheria katika mfumo wa usimamizi na utendaji wa masuala ya siasa nchini
-
Haja ya kuwa na mabadiliko ya kimfumo katika Jeshi la Polisi badala ya
ulioko sasa ambao kwa maoni ya baadhi ya watu waliozungumza na Kamati ni
wa kitaifa zaidi na kuacha serikali za mitaa bila ya wajibu wa kulinda
usalama wa raia na mali zao.
-Kwamba nguvu kubwa inatumika na vyombo vya dola/usalama dhidi ya raia na hivyo kupunguza imani ya jamii kwa vyombo hivyo.
-Kupungua kwa maadili/uzalendo miongoni mwa Watanzania kuanzia viongozi hadi wananchi hususan kwenye shughuli za kisiasa.
-Haja
ya kusisitiza elimu ya uraia kwa jamii kuanzia kwa watoto hadi kwa watu
wazima hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi ili kujenga umoja wa
kitaifa.
-Kuwepo kwa mikutano na maandamano ya vyama vya siasa yasiyokuwa na kikomo.
-Muonekano wa Jeshi la Polisi mbele ya jamii.
7.0. MATOKEO YA UCHUNGUZI KUTOKANA NA HADIDU ZA REJEA
7.1
Kuhusu “Uhalali wa mkusanyiko ulioitishwa na CHADEMA eneo la Nyololo,
Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa tarehe 02 Septemba 2012 na kuwepo
uvunjifu wa amani”, uchunguzi wa Kamati umebaini yafuatayo:
Tarehe
30 Agosti 2012 CHADEMA iliandika barua, Ofisi ya Mkuu wa Polisi Wilaya
ya Mufindi kutoa taarifa kuhusu ratiba ya mikutano ishirini na sita (26)
kwenye majimbo ya Mufindi Kusini na Kaskazini tarehe 02-03 Septemba
2012. Awali ratiba ya mikutano hiyo ilikubaliwa, lakini baadaye siku
hiyo ya tarehe 01 Septemba 2012 mikutano hiyo ilisitishwa kwa barua
Kumb. Na MFG/A.24/9/54 kutokana na kuongezwa siku za zoezi la Sensa ya
watu na Makazi hadi tarehe 08 Septemba 2012.
CHADEMA
walikataa kusitisha ratiba ya mikutano hiyo kama inavyothibitishwa na
Justin Leornard Mpotwa Katibu wa Wilaya ya Mufindi kwa barua yake Kumb.
Na CDM/M4/002/Vol.01/2012 ya tarehe 01 Septemba 2012 kuwa “pia tunaomba
ieleweke bayana kwamba kisheria shughuli zetu hazina mwingiliano na wala
kuhusiana na program iliyoongezwa ya Sensa. Kwa barua hii tunakuarifu
kuwa mikutano tuliyokutaarifu kuifanya kuanzia kesho tarehe 02 septemba
2012 itaendelea kama ilivyopangwa – CHADEMA VEMA”.
Aidha
kuwepo kwa zuio la mikutano ya Siasa ya CHADEMA Mkoani Iringa wakati wa
zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linathibitishwa na Amri ya Utendaji
(Operation Order) ya Kamanda wa Polisi Mkoa (SACP Michael Kamuhanda) ya
tarehe 01 Septemba 2012. Amri ya Utendaji ambayo ni amri halali
ilitolewa ili “kuzuia shughuli za Siasa (mikutano na maandamano) kipindi
cha zoezi la kitaifa la Sensa kuanzia tarehe 25 Agosti 2012 hadi 08
Septemba 2012”. Uhalali wa Amri/Zuio hili ulithibitishwa pia na Msajili
wa Vyama vya Siasa nchini katika barua yake Kumb Na. DA. 112/ 123/ 01/
34 ya tarehe 28/08/2010 na wakati wa mahojiano na Kamati ya uchunguzi
tarehe 22 Septemba 2012.
Licha
ya zuio/amri hii Viongozi wa CHADEMA walikataa kutii amri hiyo.
Kutokana na taarifa hizi, Kamati ya Uchunguzi inathibitisha kwamba
hapakuwepo na uhalali wa mkusanyiko/mkutano ulioitishwa na CHADEMA eneo
la Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa tarehe 02 Septemba 2012.
Kuhusu kuwepo kwa uvunjifu wa amani Kijijini Nyololo tarehe 02 Septemba
2012 Kamati ya Uchunguzi ilibaini mambo yafuatayo:
-Tukio
la kuuawa kwa Daud Mwangosi jioni ya tarehe 02 Septemba 2012 lilitokea
baada ya Operesheni ya Jeshi la Polisi kumalizika. Hii ni kwa mujibu wa
maelezo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia Mkoa wa Iringa na Joseph Senga Mpiga picha/Mwandishi Tanzania
Daima.
-
Kitendo cha kutotii amri halali ya Kamanda wa Polisi kuagiza wafuasi wa
CHADEMA watawanyike kutoka kwenye eneo la ofisi ya Kata ya CHADEMA
ilikuwa chanzo cha vurugu.
Uamuzi
wa CHADEMA kung’ang’ana kukusanyika isivyo halali eneo la Nyololo
ikizingatiwa kuwepo kwa ujumbe wa SMS kutoka kwa Dkt. Slaa, Katibu wa
CHADEMA uliosema, “IGP nasubiri simu yako. Wajulishe Polisi wako waandae
risasi za kutosha, mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji na
kisha kusherehekea, mjiandae kwa kwenda mahakama ya Den Hague. Ni
afadhali tufe kuliko manyanyaso haya”. Dr. Slaa. : ujumbe huu ukiashiria
umwagaji wa damu ni ushaidi tosha kuwepo kwa uvunjifu wa amani. CHADEMA
ndiyo Chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani Kijijini Nyololo tarehe 02
Septemba 2012.
7.2
Kama yalikuwepo makubaliano kuhusu mikutano ya hadhara au maandamano
nchini katika kipindi cha Sensa. Katika kuzungumzia hoja hii tukianzia
na Uongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi
Taifa, Kamati ya Uchunguzi ilithibitisha kuwepo kwa maagizo ya
kusimamisha mikutano/maandamano ya Vyama vya Siasa wakati wa kipindi cha
Sensa ya Watu na Makazi yaliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa
nchini, na kuongezwa muda wa Sensa hadi tarehe 08 Septemba 2012 na
Kamishna wa Sensa hapo tarehe 01 Septemba 2012.
Aidha
hoja hii imethibitika kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwa
barua yake yenye Kumb Na DA. 112/ 01/ 34 ya terehe 28 Agosti 2012 kwenda
kwa Makatibu Wakuu wa Vyama vya Siasa akiwasihi kusimamisha shughuli
zote za mikutano na maandamano ya Vyama vyao kwa kipindi chote cha Sensa
ya Watu na Makazi. Aidha kwa mujibu wa Gazeti la Serikali Na 29 VOL 93
ya tarehe 20 Julai 2012, Mhe. Rais, JAKAYA MRISHO KIKWETE kwa mamlaka
aliyopewa chini ya kifungu namba 14 cha Sheria ya Takwimu sura 351
alielekeza kwamba Sensa ya Watu na Makazi itafanyika kuanzia tarehe 26
mwezi wa nane, mpaka tarehe 08 mwezi wa tisa mwaka 2012.
Kamishna
wa Sensa aliratibu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kumalizika ifikapo
tarehe 01 Septemba 2012. Hata hivyo kutokana na tathmini aliyofanya,
kazi hiyo ilikuwa imekamilika kwa asilimia 95%. Hivyo tarehe 01 Septemba
2012 alitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari kwamba ili kila mwananchi
apate nafasi ya kuhesabiwa watu watakaokuwa wamesalia ambao ni chini ya
5% wanaombwa kutoa ushirikiano ili zoezi hili likamilike. Hivyo, wale
wote mmoja mmoja waliobakia wataendelea kuandikishwa hadi tarehe 08
Septemba 2012.
Kwa
upande wake Inspekta Jenerali wa Polisi kwa ujumbe wa simu Kumb Na
S8.7/ 2/ A/ VOL XIV/ 59 ya tarehe 28/08/2012, pia simu yake Kumb Na
C.28/ B/ 44 ya terehe 01/ 09/ 2012 aliwaelekeza Makamanda wa Polisi wa
Mikoa kutoruhusu mikutano na maandamano wakati huu wa zoezi la Sensa ya
Watu na Makazi mpaka litakapokamilika tarehe 08 Septemba 2012.
Kimsingi
Kamati ya uchunguzi imethibitisha kwamba maelekezo kwa Vyama vya Siasa
kutoendesha shughuli za mikutano ya hadhara au maandamano yalitolewa kwa
mujibu wa Sheria.
7.3
Mazingira yaliyosababisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu iliyosababisha,
kifo cha marehemu Daud Mwangosi na wengine kuumizwa, na uwiano wa nguvu
hiyo na tukio.
Hoja
kuwa Polisi walitumia nguvu kubwa katika kudhibiti mkutano wa CHADEMA
iliungwa mkono na Viongozi wa Serikali ya Kijiji, Viongozi wa dini na
Viongozi wa siasa Kijijini Wilayani na Mkoani pamoja na Waandishi wa
Habari. Hata hivyo Kamati za Ulinzi na Usalama Wilaya na Mkoa na
Viongozi wa Jeshi la Polisi waliona nguvu hizo ni za mazingira ya hali
ilivyokuwa.
Uchunguzi
wa suala hili umebaini kwamba tarehe 02 Septemba 2012 muda wa saa 10 za
jioni huko eneo la Sokoni, Kijiji cha Nyololo kulikuwepo na mkutano
usio halali ulioandaliwa na viongozi wa CHADEMA. Upo ukweli kwamba
uongozi wa Polisi ulitoa ilani kuamuru wafuasi wa CHADEMA waliokuwepo
mkutanoni hapo waondoke la sivyo nguvu itatumika. Walikaidi amri hiyo na
ilipoagizwa viongozi wakamatwe ndipo walianza kurusha mawe kwa Askari
Polisi. Baadhi ya Askari walijeruhiwa, akiwamo G 9934 PC Mgaka alivunjwa
mkono wa kulia. Pia kofia (helmet) tatu ziliharibiwa.
Kutokana
na hali hiyo amri ya kupiga mabomu ya machozi na ya kishindo ilitolewa,
kwa mujibu wa Kifungu 77 hadi 79 cha Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 – R.E
2002. Operesheni hii ilimalizika baada ya kukamatwa viongozi na wafuasi
wa CHADEMA jumla yao saba.
Baada
ya zoezi hilo kukamilika Askari Polisi walioshiriki kwenye Operesheni
waliamriwa kuingia katika magari tayari kwa kuondoka. Wakati Askari
wakipanda kwenye magari kishindo kikubwa kilitokea umbali wa zaidi ya
mita 100 kutoka sehemu ambayo operesheni ilikuwa inafanyika na
iligundulika kwamba kishindo kile kimesababisha kifo cha Mwandishi wa
Habari Daud Mwangosi.
Upelelezi
wa awali pamoja na picha za mnato unaonyesha kwamba marehemu alikuwa
amemkumbatia Mkuu wa Polisi Kituo cha Mafinga ASP Assel Mwampamba na
huku akiwa amezungukwa na Askari Polisi wasiopungua sita ambao licha ya
kumzunguka marehemu Daud Mwangosi kuna madai yaliyotolewa na mwandishi
wa Habari Joseph Senga kwamba, Askari Polisi hao walikuwa wanamshambulia
marehemu kwa kumpiga, ndipo askari mmoja aliyetambuliwa kuwa ni G 2573
PC Pasificus Cleophace Simon alifyatua Bomu la kishindo na kusababisha
kifo cha Daud Mwangosi.
Tukio
hili linaweza kugawanyika katika sehemu mbili: sehemu ya kwanza ni
wileamapamebas(mni ya kutawanya watu na ya pili ni ile ya mauaji ya Daud
Picha Namba 15: Askari Polisi wakimpiga Marehemu Daud Mwangosi, huku
OCS M wenye kifimbo) akijaribu kuwazuia. Mwangosi. Katika tukio la
kwanza idadi ya Askari walioshiriki ni Sekisheni Tukio hili linaweza
kugawanyika katika sehemu mbili: sehemu ya kwanza ni lile ya Operesheni
ya kutawanya watu na ya pili ni ile ya mauaji ya Daud Mwangosi.
Katika
tukio la kwanza idadi ya Askari walioshiriki ni Sekisheni tatu ambapo
ni askari wasiozidi thelathini. Kwa maelezo yaliyotolewa na Mwandishi wa
Habari mbele ya Kamati, Bw Joseph Senga anaeleza kuwa watu
walishatawanyika na hali kutulia mara baada ya Operesheni hii kukamilika
na Polisi kujiandaa kuondoka kwenye eneo la tukio. Tukio la mauaji ya
Daud Mwangosi lilisababishwa na kupigwa bomu la kishindo.
Maswali
ya kujiuliza katika tukio la mauaji ni Je, kulikuwepo na uwiano
unaolingana na tukio hili?, Je Palikuwa na uhalali wa kutumia Bomu la
kishindo?, na Je, utumiaji wa Bomu hilo ulikuwa na umuhimu?
Kulingana na tukio lenyewe majibu ya maswali hayo ni kama ifuatavyo:
-Hapakuwa
na uwiano wa Bomu na tukio la mauaji, kwa vile utaratibu wa matumizi ya
bomu hilo unaelekeza kulenga juu usawa wa nyuzi 45 na umbali mita 80
mpaka mita 100.
-Hapakuwa na uhalali wa kutumia Bomu la Kishindo kwani lengo la ulipuaji wake ni ili watu waogope na kukimbia.
-
Hapakuwepo umuhimu wa kutumia Bomu la Kishindo kwa sababu hata ingekuwa
ukamataji tayari Askari Polisi wapatao sita walikuwepo eneo la tukio.
Kwa
misingi hiyo Kamati imeona kwamba nguvu iliyotumika mwanzo hadi
kumaliza Operesheni haikuwa kubwa. Kuhusu tukio la kuuawa Bw. Daud
Mwangosi na kuumizwa baadhi ya Askari Polisi halikustahili kabisa.
7.4
Madai ya kuwepo uhasama kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Mkoa wa
Iringa na chanzo cha uhasama huo. Aidha madai ya kuwepo kwa orodha ya
waandishi watatu (3) ambao Jeshi la Polisi limepanga kuwashughulikia.
Katika
kupata ukweli wa jambo hili, Kamati ilikutana na wanachama wa Klabu ya
Waandishi wa Habari Iringa na pia iliwahoji Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Iringa, Michael Kamuhanda, Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, Nyigesa Ramadhani
Wankyo na Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia mkoani Iringa Said
Abdallah Mnunka.
Pia,
wakati Kamati inakutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, ilileta
suala la mahusiano kati ya Polisi na waandishi wa habari na watendaji
wakuu wa serikali wa mkoa wa Iringa.
Katika
mkutano na waandishi wa habari, ilionekana kuwa katika thathmini yao
uhusiano kati yao na Polisi hapo mkoani ni mbaya sana. Walieleza matukio
kadhaa ya kunyanyaswa waandishi wa habari wakati wapo kazini, ikiwamo
kupigwa, kutishiwa kuharibiwa na kuharibiwa vifaa vyao vya kazi na hata
kutishiwa maisha ili wasiripoti mambo ambayo Polisi wana maslahi nayo.
Kwa
mfano, mwandishi wa habari wa Star TV, Oliver Moto alieleza Kamati
kuwa: “Waandishi wa habari hawana mahusiano mazuri na Jeshi la Polisi,
na hata wanapofika ofisi za Polisi huwa hawapewi ushirikiano. Kutokana
na uhusiano mbaya wanahabari walifanya maandamano tarehe 06 Machi 2012
kupinga unyanyasaji wanaofanyiwa na Jeshi la Polisi hapa Iringa”.
Mwandishi
mwingine wa habari Zulfa Shomari ambaye anaandikia gazeti la Mwananchi
alieleza kuwa kuna matukio kadhaa ambayo Polisi wamewazuia waandishi
kufanya kazi zao mojawapo ni lile ambalo Polisi walikataza kupigwa picha
tukio la kukamatwa kwa pembe za ndovu.
Kamati
pia iielezwa na mwandishi wa habari wa ITV, Bw. Laurian Mkumbata mkasa
wa kuvunjwa kamera yake na OCD Iringa kwenye tukio moja. Ilibidi OCD
alipe kamera hiyo kwa maagizo ya RPC.
Pia
walisema kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa hivi sasa ana mawasiliano duni
sana na waandishi wa habari na juhudi za wengi wao kumfuata ili
athibitishe tukio zimekuwa zikishindwa kwani ameweka maagizo getini kuwa
mtu yeyote ambae anataka kumuona ni lazima aeleze anataka kumuona kwa
sababu gani ndipo aruhusiwe kuingia. Kwa sababu hii waandishi wa habari
wengi wamekata mguu kwenda ofisini kwake.
Mwandishi
mmoja wa Ebony FM Bw. Raymond Francis, aliiambia Kamati kuwa yeye
binafsi alitishiwa kuuawa na baada ya kuandaa kipindi kuhusiana na watu
wanaoshukiwa kufanya biashara haramu ya madawa ya kulevya ambao
wanahusiana na baadhi ya Polisi wasio waadilifu.
Mwandishi
wa Habari Greyson Mgoi wa gazeti la Kwanza Jamii aliiambia Kamati kuna
tukio la kuanguka kwa lori la mafuta eneo la Ifunda karibu na Mafinga
ambapo waliwakuta wananchi na polisi wakichota mafuta kutoka kwenye hilo
gari.
Alisema
kuwa waliamua kupiga picha tukio hilo lakini Polisi waliwakamata na
kuwalazimisha wafute hizo picha walizopiga. Kwa kuogopa shari walikubali
kuzifuta na wakaruhusiwa kuendelea na safari yao.
Waandishi
wa Habari hata hivyo walibainisha kuwa uhusiano wao na Polisi hapo
mkoani ulikuwa mzuri sana kipindi cha uongozi wa RPC Advocate Nyombi.
Walisema kuwa wakati wa RPC Nyombi, alikuwa na utaratibu wa kukutana na
waandishi wa habari na pia alikuwa anafikiwa na waandishi wa habari kwa
urahisi kwa simu au ofisini kwake. Walisema lakini ulianza kuharibika
alipohama na nafasi yake kuchukuliwa na RPC Mangara na kuwa mbaya zaidi
alipokuja Kamuhanda. Walidai kuwa Polisi wa Iringa si waadilifu na
wamekuwa wakijiona kama miungu watu.
Waandishi
walieleza Kamati, kitu kilichowaudhi sana ni yale majibu yaliyotolewa
na RPC baada ya mauaji ya Daud Mwangosi ambayo yalionekana yalikuwa ni
ya kupanga ili ukweli usijulikane. Walisema kama si picha zilizotolewa
na waandishi wa habari waliokuwepo kwenye tukio, hawadhani kama umma wa
Watanzania wangepata ukweli wa tukio hilo.
Walisema
tarehe 06 Machi 2012, walifanya maandamano ili kupinga manyanyaso ya
Polisi wa mkoani Iringa yaliyopokelewa na Mkuu wa Mkoa. Waandishi wa
Habari mkoani Iringa pia walionyesha masikitiko yao kuwa tangu kutokee
kwa mauji ya Daud Mwangosi, hawajapokea pole kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na
watendaji wake wa juu hata kama ni ya “kinafiki”.
Kwa
upande wa pili, yaani Jeshi la Polisi, Kamati ilipata taswira tofauti.
RPC Kamuhanda alisema kuwa yeye anaona mahusiano ya Polisi na waandishi
wa habari kwa ujumla ni mzuri na yeye binafsi amekuwa akikutana na
waandishi wa habari takriban kila siku asubuhi saa nne kuwapa habari.
Pia aliiambia Kamati kuwa waandishi wa habari walishiriki kikamilifu
katika kuripoti michuano ya mpira ya Kikombe cha Kamuhanda yaliyofanyika
mjini Iringa.
Msimamo
huo pia ulichukuliwa na viongozi wa juu wa kiutawala akiwemo Mkuu wa
Mkoa Dkt. Christine Ishengoma, Katibu Tawala wa Mkoa Bibi Getrude Mpaka
ambao walisema kuwa hapakuwa na uhasama wowote kati ya Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa na Waandishi wa Habari. Wote wawili walisema kuwa walimfahamu
marehemu Daud Mwangosi na aliteuliwa katika kamati kadhaa za kimkoa
ikiwa ni pamoja na ile ya kuandaa Sensa ya Watu na Makazi Mkoani, Kamati
ya Masuala ya Katiba ya Mkoa na Kamati ya Kukuza Utalii ya Mkoa.
Kuhusiana
na hisia kuwa Mkuu wa Mkoa na watendaji wake hawakujumuika na waandishi
katika msiba wa Daud Mwangosi, Dkt. Ishengoma alisema si kweli
hawajatoa rambirambi zao kwa kifo cha Mwangosi lakini alitoa pole kwa
waandishi wakati ameenda na IGP Mwema kijijini Nyololo na pia kupitia
radio katika kipindi kilichotayarishwa na mwandishi wa habari Francis
Godwin.
Baada
ya kuongea na pande hizo mbili, Kamati imebaini kwamba kuna walakini wa
mahusiano kati ya waandishi wa habari na baadhi ya askari polisi mkoani
Iringa. Kuhusu madai ya kuwepo kwa orodha ya waandishi watatu (3) ambao
jeshi la polisi limepanga kuwashughulikia.
Kwenye
tukio la Nyololo ambapo mwandishi wa habari Daud Mwangosi aliuawa,
mwandishi wa habari mwengine Godfrey Mushi alipigwa na Polisi na
inasemekana kujeruhiwa vibaya na baadaye kukamatwa na Polisi.
Kwa
mujibu wa Joseph Senga mpiga picha/mwandishi wa habari wa gazeti la
Tanzania Daima ambaye alikuwepo kwenye tukio na kupiga picha, alimuona
marehemu akipita nyuma ya gari moja la Polisi ambalo lilikuwa na baadhi
ya wanachama wa CHADEMA. Punde tu alimwona mtu amezungurukwa na askari
akipigwa lakini hakujua ni nani na yeye aliendelea kupiga picha tukio
hilo mpaka nae alipokamatwa na Polisi watatu ambao walimwuliza kama nae
anataka aende kuungana na mtu anayepigwa pale.
Senga
alisema wakati kipigo kinaendelea, kuna askari mmoja mwenye nyota tatu
(OCS Mwampamba) aliteremka kutoka kwenye gari na kwenda pale ambapo Yule
mtu aliyekuwa anapigwa huku akiwaambia “mwachieni, mwachieni, namfahamu
mimi huyo ni mwandishi wa habari!”
Senga
alisema mara alisikia kishindo kikubwa na wale askari ambao walikuwa
wanamshikilia walikimbia ndipo yeye akaendelea kupiga picha sasa za
marehemu Daud Mwangosi ambaye alikuwa amekwisha sambaratishwa na bomu.
Alieleza kuwa alimsikia yule askari ambaye alikuja kumsaidia marehemu
Mwangosi akisema “afande wameniuwa”, “afande wameniuwa”, akimwambia RPC
ambaye alikuwa karibu nae kwani nae aliumizwa vibaya katika mlipuko huo.
Senga aliiambia Kamati wale wote ambao walikuwa wame mzunguka marehemu
kama wanavyoonekana kwenye picha alizopiga walikuwepo wakati anapigwa.
Maelezo
ya Bw. Senga yanatofautiana sana na yale yaliyotolewa na RPC na OC FFU
kuwa Marehemu alimvamia OCS Mwampamba na kuwa wale askari huenda
walidhania kuwa mkubwa wao alikuwa amevamiwa ndipo walipoamua kwenda
kumsaidia. OCS Mwampamba mwenyewe wakati akihojiwa na Kamati ilipokuwa
Mafinga alisema hakumbuki kitu.
Hata
hivyo, kwa maelezo ya Bw. Senga, ambayo yanakubaliana na yale ya RPC na
OC-FFU, kitendo cha kupigwa na mauaji ya marehemu Daud Mwangosi
kilitokea baada ya kuisha ile operesheni ya kusambaratisha mkutano wa
CHADEMA na hapakuwa na mabishano yeyote au purukushani iliyotokea kabla
ya marehemu kuzungukwa na kuanza kupigwa.
Kwa
minajili hii basi Kamati imeshindwa kubaini baada ya kumalizika
operesheni na askari Polisi kuanza kuondoka, kwa nini Mwangosi
alishambuliwa kwa kipigo kabla ya kulipuliwa na bomu la kishindo?
Kwa
nini kuna maelezo yanayokinzana kati ya Bw. Senga ambaye alikuwa karibu
sana na tukio na yale ya RPC na OC-FFU ambao katika maelezo yao kwa
Kamati walisema kuwa wao walikuwa mbali kidogo na tukio kwa hiyo
hawakuweza kuona kwa dhahiri kilichotokea. Maelezeo ambayo yalirudiwa na
viongozi wa juu wa Polisi ikiwa ni pamoja na Kamishna wa Upelelezi
(DCI) Robert Manumba na Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema katika
mahojiano na Kamati.
Uchunguzi
wa Kamati haukuweza kupata ushahidi wa kubainisha kama kupigwa kwa
waandishi hao kulitokana na njama yeyote ya Polisi kuwashughulikia au
ilitokea kwenye purukushani ya vurugu zilizotokea baada ya FFU kuamriwa
kutawanya wanachama wa CHADEMA.
Pia
Kamati haikupata ushahidi wowote wa kuonyesha kuwa mauaji ya Daud
Mwangosi yalikuwa ni ya kupangwa. Kutokana na maelezo ya hapo juu,
Kamati inapendekeza yafuatayo:-
-Taasisi
za habari zinazosimamia maadili na weledi wa vyombo vya habari, hususan
Baraza la Habari Tanzania na Jukwaa la Wahariri wafanye utaratibu
unaostahiki za upatanishi kati ya waandishi wa habari, Jeshi la Polisi
na uongozi wa mkoa wa Iringa. Hii itasaidia kurejesha uhusiano mzuri
kati ya vyombo hivyo muhimu katika mkoa;
-Waandishi wa habari wapewe mafunzo ya jinsi ya kuripoti matukio ya hatari/ghasia;
-Waandishi wa habari wavae vivazi maalum vya kuwatambulisha wakiwa katika matukio hasa kwenye maeneo hatarishi;
- Waandishi wa habari wafanye kazi kwa weledi, uadilifu, uwazi na wasijibainishe na vyama vya siasa;
- Polisi ambao walihusika katika kumpiga marehemu Daud Mwangosi kabla hajauawa wachukuliwe hatua stahiki za kisheria;
-
Kamati ya Ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari
iliyoanzishwa mwaka 2008 ifufuliwe. Na kamati hizo ziteremke hadi kwenye
ngazi ya mkoa kama ilivyokuwa awali.
- Viongozi wa polisi wanapotoa taarifa za tukio, ziwe zimefanyiwa utafiti wa kina ili zisipotoshe jamii.
7.5
Uwepo wa Sheria, Kanuni au Taratibu zinazotoa uwezo kwa Jeshi la Polisi
kuzuia mikusanyiko inayoitishwa na Vyama vya Siasa na Mamlaka ya Rufaa
ambapo Vyama hivyo havitaridhika na amri hiyo.
Sheria
Namba 5 ya 1992 kama ilivyorekebishwa na Sheria Namba 7 ya 2009
inaratibu mahusiano ya kiutendaji kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya
Siasa. Kwa mujibu wa Sheria hii Jeshi la Polisi limepewa madaraka ya
kutoa zuio kwa maandishi na kuweka bayana sababu za kuzuia mikutano au
maandamano. Zuio aina hii ni halali kwa mujibu wa Sheria na ni sherti
Chama cha Siasa kiheshimu na kutii. Fungu la 11 vifungu vidogo Na 1, 4,
5, 6, 7 na 8 ya Sheria ya Vyama vya Siasa likisomwa pamoja na mafungu
Namba 43, 44, 45 na 46 ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Auxiliary Forces
Act Sura 322 vitatumika kusimamia uendeshaji mikutano ya Vyama vya Siasa
ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pamoja
na kwamba Vyama vya Siasa vinatakiwa kutoa taarifa na siyo kuomba
idhini, Jeshi la Polisi limepewa uwezo na madaraka juu ya mikutano hiyo
kuhusu kuzuia au kuruhusu na au kutoa maelekezo stahiki, kama vile
kupendekeza, na kushauri eneo mbadala na tarehe tofauti ya kufanya
mikutano/maandamano.
Aidha kutotii amri/zuio ya Jeshi la Polisi ni kosa la Jinai kwa mujibu wa Fungu la 74 la Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura 16 RE.
Vilevile
kwa mujibu wa Fungu la 43 (6) ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Auxiliary
Forces Act, Waziri wa Mambo ya Ndani ndiye Mamlaka ya Rufaa dhidi ya
amri/zuio linatolewa na Jeshi la Polisi.
Pamoja
na kuwepo kwa Sheria hizi mbili bado kuna mapungufu katika uendeshaji
na usimamizi wa shughuli za Siasa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Kwa
mfano pamoja na madaraka aliyonayo Msajili wa Vyama vya Siasa ya
kukifuta Chama cha Siasa kwenye rejesta ya usajili kwa mujibu wa Fungu
la 19 na 20 ya Sheria ya Vyama vya Siasa, kusimamisha utoaji wa ruzuku
na matumizi yake, uratibu wa shughuli za vyama hivyo hauko mikononi
mwake.
Wadau
wanashauri umuhimu wa kuimarisha uhusiano katika shughuli za utendaji
kati ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi ili
kudumisha utulivu na amani na utii wa sheria bila shuruti kwa upande
mmoja na kukuza mfumo wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa kwa upande
mwingine.
7.6 Hali ya mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa nchini katika utendaji kazi wao na Utii wa Sheria.
Kamati
ya Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel Ten, Daud
Mwangosi katika kupata majibu kwa hadidu hii ya rejea, ilizungumza na
viongozi wa vyama vya siasa kutoka ngazi za Kijiji cha Nyololo, Wilaya
ya Mufindi, Mkoa wa Iringa na Viongozi wa kitaifa jijini Dar es Salaam
na viongozi wa dini kutoka ngazi za Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya
Mufindi na Mkoa wa Iringa.
Kwa
ujumla, kila kiongozi wa chama cha siasa wa ngazi zote ambaye Kamati
imezungumza naye kuhusu hadidu hii ya rejea, ameelezea umuhimu wa Jeshi
la Polisi katika kulinda usalama wa raia na mali zao na wangependa jeshi
hilo liachwe huru katika kutekeleza majukumu yake bila ya kuingiliwa na
wanasiasa ili lifanye kazi zake kwa weledi na uadilifu.
Hata
hivyo taswira iliyojitokeza ni kwamba kuna mgawanyiko wa mtizamo kuhusu
jinsi Jeshi la Polisi linavyoshughulikia mikutano/maandamano ya Vyama
vya Siasa.
Baadhi
ya viongozi wa vyama vya upinzani wanaamini kuwa Jeshi la Polisi
linakipendelea Chama cha Mapinduzi na kubinya vyama vya upinzani, huku
viongozi wa CCM kutoka ngazi ya kijiji hadi Taifa wakilisifia Jeshi hilo
kuwa linafanya kazi yake vizuri na kwa weledi mkubwa.
Mgawanyiko
wa taswira kuhusu madai kuwa Jeshi la Polisi kuipendelea CCM hauko tu
kati ya vyama vya upinzani na CCM bali pia kwa viongozi wa dini kuanzia
ngazi za kijiji, wilaya hadi mkoani Iringa kwa maelezo kuwa hawajasikia
hata siku moja mtu anauawa na Polisi kwenye mkutano wa CCM. Mwandishi
mmoja alitoa udadisi wake kuwa huwa wanapata shida sana kuandika habari
za mikutano ya CHADEMA kutokana na jinsi Polisi wanavyojipanga kwenye
mikutano ya chama hicho.
Kudhihirisha
umuhimu wa Jeshi la Polisi katika jamii, hata wale wanaolituhumu kuwa
linakipendelea CCM, katika kutoa maoni yao kuhusu hatua za kuchukuliwa
askari wanaoharibu sifa ya Jeshi hilo, wanapendekeza kuwa askari
wahusika wachukuliwe hatua na kuomba Jeshi hilo liendeshwe kwa weledi
hasa inapotokea askari akalazimika kutumia silaha kukabiliana na fujo
isifikie kuua.
Kwa
mfano, Mchungaji Peter Katanga wa Revival Baptist Church, alishauri
chombo cha Polisi kisitumike kufanya mauaji, au kisitumike na mtu, watu,
au kikundi chochote kufanya matendo yasiyo mazuri kwa jamii kwa sababu
chombo hicho kipo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia wote na mali zao.
Viongozi
wa siasa wengine bila kujali itikadi zao, wameonekana kukerwa sana na
tabia ya watu kuuawa wakati Jeshi la Polisi linatuliza ghasia na hii
ikiachiwa iendelee inaweza kuleta uvunjifu wa amani katika nchi. Kwa
mfano, Mchungaji wa Kanisa la EFATA Nyololo, Mkombozi Kiliwa alishauri
Polisi watumie njia zinazofaa kukabiliana na wanaovunja sheria na si
kuua.
Pia
Mwalimu wa Shule ya Msingi Nyololo, Obby Kimbale, alielezea
kutokukubaliana kwake na kitendo cha mauaji ya Daud Mwangosi,
alipendekeza elimu ya uraia itolewe kwa jamii nzima vikiwemo vyombo vya
dola, viongozi wa serikali, wanasiasa na wananchi kwa ujumla wao ili
kila mtu kwa nafasi yake akaelewa namna ya kutimiza wajibu wake ndani ya
mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.
Kwa
upande mwingine, wengi waliotoa maoni yao juu ya mahusiano ya Polisi na
vyama vya siasa, pamoja na kulaumu Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa
katika kukabiliana na wafuasi wa CHADEMA, pia waliwalaumu viongozi wa
chama hicho, kwa kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi hatimaye
kusababisha Polisi kutumia nguvu kiasi hicho.
Kitendo
cha kuuawa kwa Mwandishi wa Habari, Daud Mwangosi na tabia ya kutokea
mauaji katika mikutano ya CHADEMA kimeonekana kuwakera viongozi wengi wa
vyama vya siasa kwani wanaamini kuwa Polisi huwa wanatumia nguvu kubwa
kupita kiasi ‘wanapotuliza ghasia’ katika mikutano ya CHADEMA.
Katibu
wa CCM Wilaya ya Iringa, Zakaria Mwansasu alielezea sababu ya matukio
ya namna hii kuwa ni kutokana na mmomonyoko aliouita mkubwa wa maadili
hasa katika vyama vya siasa na akashauri viongozi wa vyama vya siasa
wakapewa elimu ya uraia.
Maoni
mengi ya viongozi wa vyama vya siasa yamejikita zaidi katika hofu ya
nchi kuingia kwenye vurugu na kutoka kwenye kisiwa cha amani na hivyo
kutoa uashauri kwa viongozi wa vyama vya siasa na Jeshi la Polisi kuweka
mbele maslahi ya taifa.
Mchungaji
Yokonia Koko wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
alielezea ukosefu wa maadili kwa baadhi ya askari Polisi kuwa umetokana
na jeshi hilo kuajiri vijana ambao hawana maadili na kwamba watuhumiwa
wa mauaji kwenye matukio yanayolihusisha Jeshi la Polisi wakati wa
kuzuia fujo katika mikutano/maandamano ya vyama vya siasa wachukuliwe
hatua kali ili iwe fundisho kwa askari wengine.
Kasi
ya CHADEMA kuendesha mikutano katika sehemu mbalimbali nchini kwa ajili
ya kujiimarisha kichama, imepokewa kwa hisia tofauti na vyama vingine
vya siasa. Wakati kuna makundi ya watu katika jamii wakidhani kuwa hiyo
ni haki yao kama chama cha siasa kinachotaka kukua na kukubalika
kisiasa, wengine wanaiona mikutano hiyo ya hadhara ya CHADEMA kama ni
kuwapunguzia muda wa kufanya shughuli zao za maendeleo hasa baada ya
kipindi cha uchaguzi kumalizika.
Katibu
Mkuu wa CCM Wilson Mukama, alishauri kufanyiwa marekebisho kwenye
sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya mwaka 1992 itakayoweka wazi
shughuli za vyama vya siasa baada ya Uchaguzi Mkuu. Alisisitiza kuwa
shughuli za siasa baada ya Uchaguzi Mkuu zihamie bungeni kwa wanasiasa
kuhoji mipango ya maendeleo ya serikali na matumizi ya rasilimali za
nchi na wananchi waachwe wachape kazi zao za maendeleo.
Kuhusu
Jeshi la Polisi, Mukama alisema mfumo uliopo wa Jeshi hilo unalifanya
lionekane la kitaifa zaidi na kushauri libadilishwe kimuundo ili liweze
kutandaa hadi serikali za mitaa kuongeza nguvu katika mpango wa ulinzi
shirikishi ulioanzishwa na Jeshi hilo.
Mwanasiasa
John Shibuda alizungumzia mahusiano kati ya vyama vya siasa na Jeshi la
Polisi kwa kutoa lawama kwa vyama vya siasa kuwa havitoi malezi kwa
wanachama wake ambayo yatawafanya wawe waadilifu, wazalendo, waaminifu
na watiifu wa sheria.
Alisema
vyama vya siasa havina mfumo wa kujihakiki, kujikosoa na kujiwajibisha
na akapendekeza kuanzishwa kwa mfumo huo kisheria ambao utawajibisha
vyama vya siasa kwa matendo ya viongozi au wanachama wao.
Shibuda
alifafanua kwamba sheria anayopendekeza iwe na nguvu ya kutoa adhabu
kwa chama cha siasa na kwa kiongozi au mwanachama ambaye atathibitika
kuwa ndiyo chanzo cha uvunjifu wa amani.
Kuhusu
Jeshi la Polisi mwanasiasa huyo alipendekeza kufanyike kwa marekebisho
ya utendaji ili wakuu wa wilaya na mikoa waondolewe nguvu za kiutawala
ambazo huwafanya wakati mwingine kutoa maagizo ya kisiasa kwa Jeshi la
Polisi na hatimaye kulifanya Jeshi hilo lionekane linatekeleza maslahi
ya wanasiasa badala ya kuwa chombo cha kulinda amani.
Kwa
ujumla Kamati kutokana na maelezo mbalimbali ya Viongozi wa Vyama vya
Siasa na Jeshi la Polisi, imeona kuwa kuna mahusiano hafifu kati ya
baadhi ya Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi.
Kwa kuwa taasisi zote hizi ni wadau muhimu wa amani na utulivu nchini, Kamati inapendekeza:
-Kuwe
na jukwaa la mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Jeshi la Polisi na
Vyama vya Siasa ili kila upande ujue wajibu wake na wa taasisi nyingine
katika kudumisha amani ya nchi na utamaduni wa kuheshimu sheria zilizopo
na kupunguza migongano.
-Kuhusu
madai kwamba mauaji yanayotokea nchini yaundiwe Tume, Kamati imeona
kuwa zipo sheria zinazotoa mamlaka ya kutafiti au kuchunguza endapo kuna
mashaka ya kifo hicho.
-Muundo
uliopo wa Jeshi la Polisi uangaliwe upya kisheria ili kuziba mianya
inayotoa nafasi kwa wanasiasa kulitumia Jeshi hilo kwa manufaa ya
kisiasa.
-Nafasi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kiutendaji ziangaliwe upya ili zisitumike na mhusika kwa ajili ya manufaa ya kisiasa.
-Kwa
kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwa ndiye mlinzi wa usalama wa raia
na mali zao, siasa za ubabe kwa vyama vya siasa ziepukwe kwa kuwa
zinaleta msuguano usio wa lazima na Jeshi la Polisi
8.0. MAONI NA MAPENDEKEZO:
Kutokana
na uchunguzi uliofanyika kupitia mahojiano na Viongozi wa kada
mbalimbali, kuanzia ngazi ya Kijiji, Wilaya, Mkoa hadi Taifa, Kamati ina
maoni na mapendekezo yafuatayo:
MAONI:
-Kuhusu
madai kwamba mauaji yanayotokea nchini yaundiwe tume, Kamati imeona
kuwa zipo sheria zinazotoa mamlaka ya kutafiti au kuchunguza endapo kuna
mashaka ya kifo hicho.
-Nafasi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kiutendaji ziangaliwe upya ili zisitumike na mhusika kwa ajili ya manufaa ya kisiasa.
-Kwa
kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuwa ndiye mlinzi wa usalama wa raia
na mali zao, siasa za ubabe kwa vyama vya siasa ziepukwe kwa kuwa
zinaleta msuguano usio wa lazima na Jeshi la Polisi
-Kuhusu
operesheni ya uzuiaji wa mkutano wa CHADEMA usio halali Kijijini
Nyololo tarehe 02 Septemba 2012, Jeshi la Polisi lilitekeleza wajibu
wake ipasavyo na kutumia nguvu sahihi. Operesheni iliyoandaliwa na
kufanyika ilikamilika kwa kuwatawanya watu waliofika kwenye mkutano,
kukamata baadhi ya Viongozi na wafuasi wa CHADEMA na hali ya utulivu
ilirejea kwenye eneo husika.
MAPENDEKEZO
-Mauaji
ya mwandishi wa habari Daud Mwangosi yalitokea baada ya operesheni
kumalizika, na amri ya kuondoka kwa askari eneo la tukio kutolewa na
Viongozi wa operesheni hiyo
-Jamii
wakiwemo Viongozi waelimishwe umuhimu wa utii wa sheria, kanuni na
taratibu ili kudumisha amani na utulivu hapa nchini. Viongozi wengi
walionyesha hofu ya kuliingiza Taifa kwenye machafuko makubwa na
uvunjifu wa amani iwapo jamii haitazingatia umuhimu wa kutii sheria,
kanuni, taratibu na amri halali za Mamlaka.
-Msajili
wa Vyama vya siasa afafanue majukumu ya vikundi vya Ulinzi vya Vyama
vya Siasa kama vile Green Guard, Red Brigade, Blue Guard.
-Iwepo
programu mahususi ya Elimu ya Uraia nchini ili kujenga uzalendo na
kukuza maadili ndani ya jamii wakiwemo viongozi wa kada mbalimbali. Hivi
sasa jamii inashuhudia kutoweka kwa uzalendo na kuwepo kwa mmomonyoko
wa maadili ndani ya jamii.
Njia zifuatazo zitumike:
- Elimu ya uraia iimarishwe katika mitaala ya elimu kuanzia Shule za msingi hadi Vyuo Vikuu.
- Uamuzi wa kurudisha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa vijana utekelezwe mapema.
-
Vyama vya Siasa, Madhehebu ya Dini, Tasnia ya Habari na Taasisi
zisizokuwa za Serikali zishiriki kikamilifu katika uenezi wa Elimu ya
Uraia nchini.
-
Kuhimiza uzingatiaji wa weledi katika utendaji kazi kwa mujibu wa
taaluma na miongozo inayotolewa kuleta ufanisi. Aidha elimu endelevu
sehemu za kazi itiliwe mkazo.
-Kufanya
marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya 1992 ili kuweka wazi
shughuli za Vyama vya Siasa baada ya Uchaguzi Mkuu. Lengo ni kuwa
Shughuli za Siasa zihamie Bungeni kujadili na kuhoji mipango ya Serikali
na matumizi ya rasilimali za nchi. Kwa kufanya hivyo wananchi watapata
nafasi kufanya kazi za maendeleo.
-Kuboresha
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, hususan uanzishwaji wa
ofisi ngazi ya Mkoa na Wilaya ili kuratibu ushirikiano/mahusiano baina
ya serikali (Jeshi la Polisi) na Vyama vya Siasa. Lengo ni kukuza
mahusiano na kuondoa mgongano.
-Utaratibu
wa kufanya mikutano mara kwa mara kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya
Siasa, Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari uimarishwe ili kujenga
mahusiano mazuri na kupata ufumbuzi wa haraka kwa matatizo
yaliyojitokeza.
-
Jeshi la Polisi nchini ni chombo muhimu katika ulinzi na usalama wa raia
na mali zao. Muundo uliopo wa Jeshi la Polisi uangaliwe upya Kisheria
ili kuziba mianya inayotoa nafasi kwa wanasiasa kulitumia Jeshi hilo kwa
manufaa ya Kisiasa. Aidha mipango ya kuboresha utendaji kazi kitaaluma
iliyopo hivi sasa upewe msukumo stahiki hususan rasilimali watu na
fedha.
-
Wananchi wahamasishwe kushirikiana na Polisi Jamii na Ulinzi shirikishi.
Polis ishirikiane na Serikali za mitaa kufanikisha malengo hayo.
-
Jeshi la Polisi liimarishwe ili litekeleze majukumu yake kikamilifu na
kujenga mahusiano sahihi kati yake na Jamii, Vyama vya Siasa, Tasnia ya
Habari na Asasi zisizo za Kiserikali.
-Taasisi
za habari zinazosimamia maadili na weledi wa vyombo vya habari, hususan
Baraza la Habari Tanzania na Jukwaa la Wahariri wafanye utaratibu
unaostahiki wa upatanishi kati ya waandishi wa habari, Jeshi la Polisi
na uongozi wa mkoa wa Iringa. Hii itasaidia kurejesha uhusiano mzuri
kati ya vyombo hivyo muhimu katika mkoa.
-Waandishi wa habari wapewe mafunzo ya jinsi ya kuripoti matukio ya hatari/ghasia.
-Waandishi wa habari wavae vivazi maalum vya kuwatambulisha wakiwa katika matukio hasa kwenye maeneo hatarishi.
-Waandishi wa habari wafanye kazi kwa weledi, uadilifu, uwazi na wasijibainishe na vyama vya siasa.
-Kamati
ya Ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari
iliyoanzishwa mwaka 2008 ifufuliwe. Na kamati hizo ziteremke hadi kwenye
ngazi ya mkoa kama ilivyokuwa awali.
-Viongozi wa Polisi wanapotoa taarifa za tukio, ziwe zimefanyiwa utafiti wa kina ili zisipotoshe jamii.
-Kuwe
na jukwaa la mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Jeshi la Polisi na
Vyama vya Siasa ili kila upande ujue wajibu wake na wa taasisi nyingine
katika kudumisha amani ya nchi na utamaduni wa kuheshimu sheria zilizopo
na kupunguza migongano.
9.0. CHANGAMOTO
Changamoto zilizojitokeza katika Uchunguzi zimegawanyika katika mtiririko ufuatao:-
9.1 Jeshi la Polisi:
- Ukosefu wa Mafunzo endelevu.
- Ukosefu wa Uvumilivu katika utekelezaji wa Majukumu.
-Uelewa mdogo wa Elimu ya Uraia.
- Mmomonyoko wa Maadili.
- Kukosekana kwa uzalendo.
- Ukosefu wa Utii wa Sheria, Kanuni na Taratibu
9.2 Vyama vya Siasa:
- Kukosekana kwa uvumilivu katika kuendesha shughuli za Siasa.
-Kukosekana kwa Elimu ya Uraia
- Uelewa mdogo wa baadhi ya Viongozi wa Vyama kuhusu uendeshaji wa Vyama vya Siasa.
- Ukosefu wa Sera/Mwongozo kwa Vyama vya Siasa kuendesha shughuli za Kisiasa baada ya uchaguzi mkuu.
- Kukosekana kwa Jukwaa linalokutanisha mara kwa mara Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi
- Mmomonyoko wa Maadili.
- Suala la Uzalendo.
- Ukosefu wa Utii wa Sheria, Kanuni na Taratibu
9.3 Jamii:
- Elimu ya Uraia.
- Mmomonyoko wa Maadili.
- Kukosekana kwa uzalendo.
- Ukosefu wa Utii wa Sheria, Kanuni na Taratibu.
26
10 HITIMISHO
Hayati
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uhai wake aliwahi kusema
kuwa, “ili nchi iendelee inahitaji vitu vinne ambavyo ni watu, ardhi,
siasa safi na uongozi bora. Watanzania kila mtu mahali pake, tunahitaji
kuwa na siasa safi yenye kujenga ustawi, tija, mshikamano, amani,
maendeleo na afya kwa taifa letu”.
Utulivu
na amani kwa ajili ya mustakabali wa taifa, imekuwa ni kauli mbiu ya
viongozi mbalimbali ambao Kamati hii imepata fursa ya kuzungumzia juu ya
hali ya siasa na mahusiano yaliyopo baina ya Serikali, (Jeshi la
Polisi, Kamati za Ulinzi na Usalama wilaya na mkoa), vyama vya siasa,
viongozi wa dini na wananchi.
Wananchi
na Viongozi wanataka kuona shughuli za siasa ya vyama vingi inaendeshwa
kwa hoja zenye tija badala ya vurugu na utengano. Njia mojawapo ya
kukabiliana na hali hii inayojitokeza ni kujenga uzalendo, maadili mema,
na mshikamano ili Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani na utulivu.
Kamati hii inashauri na kupendekeza kuwa maoni haya yazingatiwe na kutekelezwa.
Aidha
Kamati imefaidika sana kupata fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali
kuanzia kijiji hadi taifa na walitoa ushirikiano wa dhati katika kutoa
mchango wao wa mawazo. Kamati inapenda kutoa shukrani za dhati kwa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Dkt Emmanuel Nchimbi (Mb) kwa
imani yake kwa wajumbe wa Kamati ya Uchuguzi.Source:Mo blog
No comments:
Post a Comment